UMUHIMU WA MAOMBI KATIKA IBADA
MAOMBI
Haya ni mawasiliano
kati yako na Mungu wa Mbinguni.Na kama ilivyo kwa mawasiliano ya kawaida mfano
ya moja kwa moja, ya simu, ya barua au kwa njia nyingine yoyote maombi lazima
yawe ni majibizano(dialogue) kati ya
watu wawili au zaidi.Kama nilivyo sema katika sura zilizopita kuwa Mungu
anataka kuwe na mazingira yanayofaa(condunsive
environment) ili mtu aweze kumwabudu Mungu kwa Roho na kweli, hivyo vitu
vyote tunavyohitaji, Mungu ameshaviandaa katika ulimwengu wa Roho,uwe utajiri,
elimu, mke au mume, chakula, afya, mahali pa kuishi, kazi na mengine
yote.Hivyo, tafsiri nyingine ya maombi ni kuchukua vitu katika ulimwengu wa roho
na kuvibadilisha viwe katika ulimwengu wa mwili.Lazima utambue kila
unachokiomba kipo katika ulimwengu wa roho na inakuhitaji wewe uingie kwenye
maombi ili ukibadilishe kiwe katika ulimwengu wa mwili(halisi).
Ndio maana wakati
mfalme Hezekia alipokuwa akiongoza wana wa Israeli ilifikia wakati Mfalme wa
Ashuru alianza kuwadhihaki na kuwatukana siyo kwa sababu Mungu hakuwepo au
ushindi haukuwa wao, lakini Mungu alitaka wapitie hatua ya maombi kuomba
ushindi katika ulimwengu wa roho udhihirike kwa namna ya mwili.Tunasoma Isaya 37;3, “Wakamwambia, Hezekia asema hivi,Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu na
matukano; maana watoto wa tayari kuzaliwa, wala hapana nguvu za kuwazaa”.Maana
yake hakuna kitu kinachoweza kufanya watoto wazaliwe ingawa ndani ya tumbo
wamo.Kuna watu wengi hupata mafunuo ya aina mbalimbali kuhusu maisha yao ya
mbele au ya wengine lakini mara nyingi hayo mafunuo hayatokei kama yalivyo au
hayatokei kabisa sababu ni kwamba haukuingia kwenye maombi kwani yalikuja kwa
namna ya roho na wewe ulitakiwa uyalete katika ulimwengu wa mwili yadhihirike.
Dada mmoja aliniambia
kuwa siku mbili kabla mama yake hajafariki aliota ndoto kuhusu kifo
hicho.Akabaki tu na hofu na huzuni kusubiri hicho kifo baada ya siku hizo mbili
mama yake akafa.Sasa hii ni hatari sana unapopewa maono au ufunuo wa namna hii
maana yake wajibu wako ni kuomba hiyo roho ya mauti isiwe na nguvu juu yake ili
apewe uzima na aendelee kuishi.Na lazima unapoingia kwenye maombi uhakikishe
hautoki mpaka kitu unachoomba kinatokea(PRAY UNTIL
SOMETHING HAPPEN).Katika
kuomba kwako utakapoomba sawasawa Mungu atakupa mwongozo wa nini cha kufanya
ili ukipate kile unachokihitaji.Wakati mwingine Mungu anakuwa amekuchagua wewe
pekee ili usimamie kwa njia ya maombi kitu Fulani kitokee au kitu Fulani
kisitokee na unapokiuka na kuacha kuomba kama anavyokupa mwongozo ujue
unavuruga mfumo mzima wa kufanyika au kutokufanyika kwa hicho kitu iwe
kinakuhusu wewe au mtu mwingine lazima uwe makini sana.
Kumbuka pia maombi yako
ni kama manukato(pafyumu) mbele za
Mungu unapoomba, maana yake katika ulimwengu wa roho unafanya hali ya hewa ya
mbinguni iwe nzuri na kupendeza. “Hata
alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne
wakaanguka mbele za mwanakondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya
dhahabu vilivyojaa manukato ,ambayo
ni maombi ya watakatifu”.Ufunuo 5;8.Wakati
mwingine inatokea Baraka zinashuka juu ya nchi au familia lakini uliomba tu
kwaajili ya mambo mengine ya ufalme wa Mungu. Maombi yako yanamgusa Mungu
lakini endapo unaomba kwa utakatifu.
NAFASI YA ROHO
MTAKATIFU KATIKA MAOMBI YAKO
Roho mtakatifu ni nafsi
ya tatu ya Mungu ambapo nyingine ni Mungu Baba na Mungu mwana(Yesu).Katika kila kipindi Mungu amekuwa
akidhihirika kwa watu wake kwa namna mbalimbali.Katika Agano la kale Mungu
amekuwa akidhihirika kwa nafsi ya kwanza ya Mungu Baba.Hii tunaiona dhahiri
wakati akisema na Adamu,Nuhu, Ibrahimu, Musa, Eliya na wengine.Katika Agano
jipya kabla ya siku ya Pentekoste, Mungu amekuwa akidhihirika kwetu kwa nafsi
ya pili ya Mungu mwana(YESU) ndio
maana wakati Yesu anatarajiwa kuzaliwa malaika akamwambia Bikira Mariamu, “Hayo yote yamekuwa ili litimie neno
lililonenwa na BWANA kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, Bikira atazaa mwana;
Nao watamwita Imanueli; Yaani Mungu pamoja nasi”.Mathayo 1;22-23.
Kazi yake Yesu ilikuwa
kufanya matengenezo na urejesho wa mwanadamu kwa Mungu na kumwandaa mwanadamu
ili aweze kukaa ndani yake.Sasa baada ya Yesu kufanya kazi yake aliyotumwa
ikawa ni zamu ya Roho mtakatifu nafsi ya tatu ya Mungu kuja kukaa na mwanadamu
na kudhihirika mpaka mwisho wa dunia.Pasipo Roho mtakatifu sisi hatuwezi kamwe
kuomba itupasavyo. “Kadhalika Roho naye
hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho
mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa”.Warumi 8;26.Hivyo wakati wote ili maombi yetu yapate kibali mbele
za Mungu ni lazima Roho Mtakatifu atuongoze kuomba.Yeye anafanya kazi ya
kushuhudia kwa ulimwengu(wasiookoka)
juu ya dhambi, haki na hukumu (Yohana
16;8-11).Na kwetu sisi ambao tumeokoka Yesu anasema, “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli,atawaongoza awatie kwenye
kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayo
yasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake”.Yohana 16;13.Pia anasema katika Yohana 14:26, “Lakini huyo msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwenu
kwa jina langu, atawafundisha yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia”.
Anaposema atawafundisha
yote maana yake hata kama biashara, masomo, ndoa, uchumba, au lolote lile linakutatiza
yeye anaweza kukufundisha.Roho Mtakatifu anapokuwa ndani yako hata pumzi yako
inakuwa tofauti, inakuwa kama ya Mungu na inakuwa na nguvu sawasawa kabisa na ya
Mungu kwani Roho Mtakatifu yumo. Maana yake ukiwapulizia wagonjwa wanapata
afya,hata mtu aliyekufa anafufuka.Kumbuka kwa pumzi hiyohiyo Mbingu na nchi zilifanyika(Zaburi 33;6) na kwa pumzi Mungu
alimpulizia mtu naye akawa nafsi hai(Mwanzo
2;7).Biblia inasema, “Nasi twajua ya
kuwa katika mambo yote Mungu
hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale
walioitwa kwa kusudi lake”. Warumi
8;28.Mungu anataka afanye kazi na wewe katika kuwafanya watu wapate afya na
ufufuko miilini mwao.
Kuna mambo mawili
yanayofanya pumzi yako isipitishe NGUVU
za Mungu au isifanye kazi kama Mungu alivyokusudia.Jambo la kwanza ni
kutokufahamu juu ya inatokea nini unapomruhusu Roho Mtakatifu atende kazi
kupitia pumzi yako.Jambo la pili ni kutia unajisi katika njia au mfumo ambao
pumzi hiyo inapitia.
Yesu anasema, “Yeye aniaminiye mimi kazi nizifanyazo mimi,
yeye naye atazifanya; naam na kubwa kuliko hizo atazifanya: kwa kuwa mimi
naenda baba”.Yohana 14;12.Anaposema,
“kwa
kuwa mimi naenda kwa Baba” ,kwa maana nyingine ni kuwa kwa kuwa Roho
Mtakatifu atawashukia na kukaa nanyi.Ndio maana alisema yawafaa ninyi mimi
niondoke maana nisipoondoka huyo msaidizi(Roho
Mtakatifu) hatakuja kwenu(Yohana
16;7).Hivyo ili ufanye kazi kubwa na miujiza mikuu kwa ajili ya utukufu wa
Mungu ni lazima uwe na Roho mtakatifu ndani yako na umpe nafasi ya kutosha
kabisa ili aweze kuonesha ukubwa wa uweza wake usio na mwisho katika kutenda
miujiza.
KUNENA KWA LUGHA.
Kunena kwa lugha ni
matokeo au ishara mojawapo ya wazi ya kuwepo kwa Roho Mtakatifu ndani yako.Na
hii haimaanishi kuwa usiponena kwa lugha basi moja kwa moja hauna Roho
Mtakatifu, La hasha!!Matendo ya mitume
2;4, “wote wakajazwa Roho Mtakatifu,
wakaanza kusema kwa lugha nyingine kama Roho alivyowajalia kutamka”.Pia
mtume Paulo anasema katika 1Wakorintho
14;2, “Maana yeye anenaye kwa
lugha,hasemi na watu bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena
mambo ya siri katika roho yake”.Hivyo ni muhimu sana kwa uliyejazwa na Roho
Mtakatifu uwe na kiu na unene kwa lugha kwani ni Roho Mtakatifu anakuwa
anazungumza mwenyewe mbele za Mungu ule uhitaji halisi wa roho yako..Saa
nyingine unaponena kwa lugha unakuwa unaombea au kutamka hata mambo ambayo yako
juu ya kiwango cha imani yako lakini yanakuwa yako katika mapenzi ya Mungu
uyapate kwa wakati huo.Kwa tafsiri nyingine
tunaweza kuita MUUJIZA.Unapoomba
kwa kutumia akili mara nyingi utaomba juu ya mambo yale uyajuayo tu. Wakati
mwingine kunakuwa na jambo baya ambalo litatokea mbele yako mfano Ajali, kifo,
kufukuzwa kazi, nyumba kuungua moto, hitilafu ya umeme n.k na unakuta ndani yako unapata msukumo wa
kuomba lakini hujui uombe au uombee juu ya nini lakini kunena kwa lugha
kunakusaidia uweze kuomba au kuombea hilo tukio mbele yako na kulizuia
mapema lisitokee.
Jambo la muhimu la
kujua ni kuwa kunena kwa lugha siyo ufahamu au ujuzi anaokuwa nao mtu wa kuomba
bali ni neema ya bubujiko la Roho Mtakatifu.Hivyo, omba Mungu akupe kiu hii
kubwa baada ya kutambua umuhimu wa kunena kwa lugha ili uombe kama vile Mungu
atakavyo uombe na wala usijaribu kuigiza maana utakuwa umemdharau Roho
mtakatifu ambaye ndiye mpaji na hapohapo utafanya shetani apate mwanya wa
kukuingizia lugha bandia za mapepo.Kumbuka kuna lugha mbalimbali kama vile za
watu, wanyama, malaika, mapepo n.k. hivyo pia ni lazima uwe makini. Kunena
katika Roho Mtakatifu lazima utajisikia huru, mwepesi na pia utasikia amani ya
Mungu ndani yako.
Nafasi ya kifalme na
kikuhani katika maombi yako.
Kazi mojawapo ya KUHANI ni kuomba toba na utakaso kwa
ajili ya watu au mahali Fulani.Wakati wote wa Agano la kale Mungu amewatumia
makuhani katika maeneo yote yahusuyo toba au utakaso wowote ule.Nao ndio pekee
walioruhusiwa kuingia patakatifu pa patakatifu sehemu ya ndani kabisa ya hekalu
huku akiwa amejitakasa yeye kwanza.Baada
ya Yesu kuja Mungu akamfanya awe kuhani mkuu kwa Mungu wetu kwaajili ya dhambi
zetu.
“Maana ameshuhudiwa kwamba; wewe u kuhani milele, kwa mfano wa
Melkizedeki……………………Na kwa kuwa haikuwa pasipo kiapo, (maana wale walifanywa
makuhani pasipo kiapo bali yeye, pamoja na kiapo kwa yeye aliyemwambia ,Bwana
amwapa wala hataghairi U kuhani milele;)basi kwa kadiri hii Yesu amekuwa
mdhamini wa Agano lililo bora zaidi”.Waebrania
7;17-22.Ndio maana alipokuwa akikata roho msalabani pazia la hekalu lilipasuka vipande viwili toka chini mpaka
juu.Hii ilikuwa ishara ya kuachiliwa kwa wana wa Mungu (watakaookoka) kuingia patakatifu pa patakatifu kama makuhani.
MFALME
ni mtu ambaye anatawala na kumiliki ufalme katika eneo Fulani.Na yeye ndiye
mwamuzi wa mwisho katika hilo eneo.Maana yake akitaka kuzuia jambo Fulani baya
au zuri linalotendeka mahali hapo anaweza wala hakuna awezaye kumzuia. “Kwakuwa neno la mfalme lina mguvu, naye ni
nani awezaye kumwambia huyo, wafanya nini?”.Mhubiri 8;4.Mamlaka ya kifalme huwa inatoka kwa Mungu au kwa miungu
mingine(shetani) ndio maana hata
neno lake(mfalme) ni vigumu
kulipinga au kuzuia.
Lakini mimi nizungumzie
kwa upande wa Ufalme ambao unapewa kutoka kwa Mungu ambaye ni mfalme wa
wafalme.Neno linalotoka kwa huo ufalme linakuwa na nguvu juu ya falme na kila
mamlaka iwayo yote.
“Msiogope enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule
ufalme”.Luka 12;32.Hivyo fahamu wazi
kuwa wewe ni mfalme na umepewa
majukumu ya kifalme na Mungu
mwenyewe.Na kiwango cha kutawala na kumiliki kieneo kinategemea maamuzi yako na
utendaji wako wa kazi uliyopewa. Ufunuo
5;9-10 inasema, “……………….kwa kuwa
ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na
jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu,Nao
wanamiliki juu ya nchi”.Sema tena “Ukawafanya
kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu”. Ukikaa sawasawa katika nafasi yako
ya kifalme na kikuhani unapewa uwezo wa kumiliki nchi yaani eneo husika lenye
mipaka kamili.Hakuna haja ya kulalamika ooh!! nashindwa kuabudu kwani nyumba
yangu ipo karibu na baa au klabu ya pombe, au hakuna haja ya kufanya mgomo ili
upate haki au mshahara wako matokeo yake unapigwa na askari wa usalama na
kuumia bure.Badala yake kaa na kutulia halafu chukua nafasi ya kikuhani kwa kuomba toba kwa ajili ya
watu hao au eneo husika unalotaka hayo mabadiliko kisha, chukua nafasi ya kifalme kwa kutamka neno la kifalme la
uamuzi wa mwisho ulioamua kwa mazingira hayo kuwepo kwa njia ya maombi na Mungu
ni lazima atafanya mabadiliko.Usiombe kama vile mtu asiyestahili(mtumwa) kama mwanamke Mkananayo(Mathayo 15;21-28).Kwani Mungu
amekustahilisha kuwa mtoto wake.Yesu akawaambia, “Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo Bwana wake;
lakini ninyi nimewaita rafiki; kwakuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu
nimewaarifu”.Yohana 15;15.
Wengine wanapoomba kwa
ajili ya mtu mwenye mapepo wananyenyekea na kupiga magoti kwani hawajui nini wanakifanya
lakini nakuambia katika kazi hiyo au maombi hayo hebu kemea pepo au nguvu za
giza huku umesimama kwa ujasiri kabisa kama mfalme kwa mamlaka uliyopewa na
BWANA nakuambia pepo atachomoka bila kuleta kiburi chochote kwani anajua
unaifahamu nafasi yako uliyopewa na Mungu.
WITO.
Ikiwa umejifunza na
kutambua sasa kuwa Ibada yako haikuwa sawa mbele za Mungu au bado ndani yako
haujampokea Yesu kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yako( HAUJAOKOKA) na unataka urudi kwenye msingi wa kumwabudu Mungu
halisi katika Roho na kweli, haujachelewa.Yesu anasema, “Tazama nasimama, mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na
kuufungua mlango, nitaingia kwake nami nitakula pamoja naye(mambo yote hatatenda bila kukushirikisha),
na yeye pamoja nami”.Ufunuo 3;20.
“Kwa maana husema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu
nalikusaidia; Tazama wakati uliokubalika ndio sasa; tazama siku ya wokovu ndiyo
sasa”.2Wakorintho 6;2.
Tafuta MAHALI PA
UTULIVU na Sema sala hii pamoja nami kwa Roho na kweli kutoka ndani ya moyo
wako;
“Bwana
Yesu, ninakushukuru kwa Rehema na fadhili zako nyingi ulizozionesha pale
ulipojitoa na kufa msalabani kwa ajili yangu mimi mwenye dhambi.Ninakuja kwako,
ninaomba unisamehe dhambi zangu zote na unipokee,futa jina langu katika kitabu
cha mauti, na uliandike kwenye kitabu cha uzima; unipe uwezo wa kufanyika
mtoto wako tangu sasa. Ninajiachilia kwako,
uwe BWANA na mwokozi wa maisha yangu; unitawale katika mwili, nafsi na roho
yangu, nikatembee katika mapenzi yako siku zote za maisha yangu.Asante kwa kuwa
tangu sasa nimeokoka na kuwa kiumbe kipya. Ya kale yote yamepita na
tazama,yamekuwa MAPYA, katika jina lenye NGUVU na MAMLAKA, jina la YESU
ninaomba na kuamini kuwa nimepokea sasa.AMEN!!!
Baada ya kusema sala
hii amini kuwa upo ndani ya Yesu naye yuko ndani yako.Endelea kuishi katika
misingi ya utakatifu katika kujifunza Neno lake na maombi huku ukiufurahia UZURI wa Yesu usiochakaa ndani ya
wokovu huu aliokupa.Anasema, “ na tazama,
mimi nipo pamoja nanyi siku zote hata ukamilifu wa dahari”. Mathayo 28;20b. MUNGU AKUBARIKI!!!!
Kwa maombezi, maswali,
maoni, ushauri au kama unaguswa kuwa mwombezi maalumu kwa huduma hii, tafadhali
usisite kuwasiliana nami kwa anuani zifuatazo;
Simu namba; 0757 350 527 au 0717 236 490.
Comments
Post a Comment