SIFA.
Maana halisi ya sifa ni kumwambia au kumshuhudia
Mungu au watu matendo ambayo huyo Mungu wako ameyafanya.Hii inatokana na mguso
wa ndani ya moyo wa mtu unaompelekea aimbe kwa furaha, acheze, arukeruke na
kushangilia huku akimtaja Mungu wake na matendo ambayo ametendewa.Inawezekana
ikawa uhai, kuponywa magonjwa, kupewa nafasi nzuri kimasomo, kupata kazi,
kuinuliwa kiroho, kusamehewa n.k.Sifa ipo katika maeneo makuu mawili ambayo ni
sifa ya Mungu aliye hai au sifa kwa mashetani.
Nikianza na sifa ya Mungu biblia inasema; “Haleluya, Msifuni Mungu katika patakatifu
pake, Msifuni katika anga la uweza wake, Msifuni kwa matendo yake makuu;Msifuni
kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake…………………………….Na kila mwenye pumzi na amsifu
BWANA. Haleluya!”.Zaburi 150:1-6.Anaposema
msifuni Mungu katika patakatifu pake maana yake ni Mbinguni,mbele ya kiti chake
cha enzi au pamoja naye; ndio maana nimekwambia lazima uwe mtakatifu kwa sababu
ndipo mahali pa kumpa Mungu sifa pekee.Mungu wetu ni mtakatifu, anakaa mahali
patakatifu na lazima vyote vilivyopo karibu naye viwe vitakatifu.Kutoka 19:110-21.
Unapokuwa katika sifa
hebu sifu kama upo mbele ya Bwana mwenye NGUVU na UWEZA, usisifu
kizembekizembe.Ndio maana anasema msifuni Mungu katika anga la uweza wake, kwa
matendo yake makuu na kwa kadri ya wingi wa ukuu wake.
Wakati ule mfalme Daudi
ameshinda ile vita na Wafilisti hakujali nafasi yake kama mfalme maana alijua
kuna mfalme wa wafalme anayemsifu
ambaye ndiye hasa aliyefanya washinde na warudi na sanduku la Agano.Na Yule
mwanamke aliyetaka mfalme asisifu kwa jinsi ile alipata laana ya kutopata mtoto
maisha yake yote.(2Samweli 6:16,20-23).Usijaribu
kuzuia sifa itokayo ndani ya mtu kwaajili ya BWANA maana hakika laana itakuwa
juu yako.Sifa ya Mungu ni ya Mungu wala hakuna mtu awezaye kuchukua sehemu
yake.
Kwa upande wa sifa ya shetani watu huingia kumsifu
shetani, maovu na kazi nyingine anazofanya.Pia wengine husifu dhambi kuwa ni
kitu kizuri kufanya na ndio maana usishangae unapoona karibu asilimia tisini (90%)
ya vijana wanaoimba nyimbo za kidunia wanaimba juu ya suala la mapenzi au zinaa
wakati Mungu kasema wazi kuwa usizini wala kumtamani mwanamke(au mwanamume) asiye wako.Kinyume chake
unakuta anaimba na mtu asiye wake na
kuanza kukumbatiana na kufanyiana vitendo vya uzinzi halafu baadaye utamkuta na
mtu mwingine akiimba na kufanya mambo yaleyale.Hii ni kukaribisha Sodoma na
Gomora nyingine kwa mara ya pili.
Biblia inasema, “Wala
msiifuatishe namna ya dunia hii, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate
kujua hakika mapenzi ya Mungu, yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu”.Warumi 12:2.
Sasa watu wengi wamekuwa
wakiiga mitindo/staili za muziki ya kidunia na kuingiza katika kumwabudu Mungu
na makanisa mengi sasa hivi yamejaa machafuko haya.Na wengi hujidanganya na
kujifariji kuwa wananyang’anya kile ambacho shetani alidondoka nacho kutoka
Mbinguni.Lakini Biblia inasema, “Hivyo husema,
Alipaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa”.Waefeso 4;8 .Maana yake
ujuzi au kipawa unapewa kutoka juu yaani Mbinguni na sio kwingineko.Sasa
inashangaza kwako kusubiri ujuzi ambao shetani anawafunulia watu wake ndipo
uige.Hebu kaa utulie halafu umwambie Mungu nahitaji kukusifu kwa ustadi zaidi,
naomba unipe ujuzi, na Mungu sio dhalimu hata akashindwa kukupa,atakupa tu.
Tambua hii siri kuwa kila alama unayoijua ina maana
yake au kazi yake na hiyo kazi inaweza kuwa nzuri au mbaya.Kwa mfano mstari( ) ni nukta
iliyoendelezwa.Kuna watu hunishangaza wanapojiita majina ya ajabu mfano, “RED
DEVIL” na wala hawana shida pasipokujua kuwa wanamtukuza shetani na kuwa kuna
madhara yake tena makubwa, halafu na wewe mtu wa Mungu huoni shida hata kidogo
na unashangilia tu!!shauri yako, Mungu anaweza kukutapika.Au unafahamu ni
kwanini waimbaji wengi wa muziki wa kidunia wanaimba huku wanachomachoma mikono
yao chini(kuzimu) na huku watu wa Mungu wakiabudu wanaelekeza mikono yao juu
(Mbinguni)?
Wengi hawajui wanachokifanya lakini ninakuambia wazi kuwa
wanamwabudu Shetani kama Mungu bila kujijua.Unakuta wanapoimba vibwagizo vyao
ni, “yo!yo!yo!” au “G!G!G!” n.k.Hivi vitu au maneno vina maana kabisa na kazi
yake.Hebu omba Mungu akufunulie zaidi na kukuelewesha juu ya mambo hayo ili
upate ufahamu na maarifa.
Hosea
4:6, “Watu wangu wanaangamizwa
kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa
wewe, usiwe kuhani kwangu mimi, kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi
nami nimewasahau watoto wako”.Lazima ukifahamu kile
unachokifanya kama ni cha Mungu au cha kishetani kwa kumuuliza Mungu.Mtumishi
mmoja alisema hivi, “Je, huwa unafanya
nini unapokuwa hujui nini cha kufanya?”.Jawabu ni kwamba lazima umuulize
Mungu, usiingie kufanya halafu baadaye ukapata madhara makubwa.
Siku moja nikiwa nimelala niliota ndoto hii; “
nilikuwa na rafiki yangu mmoja mahali Fulani baada ya kuzungumza naye kitambo
akaniambia twende pamoja nikachukue kitu fulani nyumbani kwao.Tulipita kwenye
nyumba moja ambapo mimi nilipita nyuma ya ile nyumba na yeye mbele yake.Baada
ya kuivuka nikakuta Yule mwenzangu yuko mbele umbali kidogo, nikajipa matumaini
kuwa nitamkuta tu.Nikafika sehemu kuna nyumba nyingine halafu kwa pembeni kuna
msitu mkubwa.Nikawa nasikia kama kuna sauti za watu waimbao.Nikamuuliza mmoja
wa wakazi wa pale, kuna nini kinaendelea huko msituni? Akasema katikati ya huo
msitu kuna kanisa liitwalo “NGUVU YA NGOMA”.Nikageuka kutazama kwenye
mlango(mwanzo wa kuingia ndani ya huo msitu) na nikaona kuwa kulikuwa na miti ambayo juu yake kulikuwa na majitu na
kamba imeteremshwa mpaka chini, na kila apitaye ananaswa na kamba na
kupandishwa juu.Nilikuwa na wazo la kuingia nione wanaabuduje lakini nilipoona
mtu mmoja amenaswa anapandishwa juu na kamba nikaogopa.Ghafla nikajikuta nipo
nyuma ya hilo kanisa nyuma kabisa na wakati huo watu wote walikuwa mbele
wanasifu na mdundo mzito wa ngoma.Wengi wao walikuwa watoto na vijana pia
baadhi ya wazee walikuwepo.Roho wa Mungu akaniambia hilo ni moja ya makanisa
yanayotolewa kuzimu na kuletwa duniani.Lengo ni kuwateka watu hasa watoto na
vijana kwa njia ya sifa(uimbaji) waingie jehanamu”.
Ninapenda nikwambie
kuwa sifa halisi ina NGUVU kubwa na
ya ajabu.Maana yake ukimsifu Mungu utaona nguvu za Mungu hali kadhalika
ukimsifu shetani utapata nguvu zake.Inashangaza ninapoona watu(vijana) wanaimba
nyimbo na kusema, “Nakupenda mpenzi jini” au “nataka niolewe na jini” sijui
wanaelewa maana yake au wanaimba kwa lengo la kuwafurahisha
watu.Ni ajabu hasa ninapoona hata mtu uliyeokoka
unajiingiza huko na hapo ni lazima Ibada yako ivurugike hata ukatae!!
MJUE
SHETANI NA MBINU ZAKE
Kabla ya kuasi kwake shetani alikuwa ni malaika mkuu
wa sifa mbinguni na jina lake akiitwa Lusifa. “Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa
kifuniko chako……………………….kazi ya matari na filimbi ilikuwa ndani yako; katika
siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari.Wewe ulikuwa Kerubi mwenye kutiwa
mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu,
ukatembea huko na huko kati ya mawe ya moto.Ulikuwa mkamilifu katika njia zako
tangu siku ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako”.Ezekieli 28:13-15.
Baada ya kuasi jeshi
la Mbinguni wakamtupa chini kuzimu pamoja na malaika waliokuwa wameungana naye.
“………………….Lakini utashushwa mpaka kuzimu
mpaka pande za mwisho za shimo”.Isaya
14:14-15.Baada ya hapo shetani akaanza mikakati mikubwa ya kuhakikisha
mwanadamu naye anaangamia pamoja naye kwenye moto wa milele.Kwa kuanza na baba
yetu Adamu akaanza kupanua mtandao na mbinu mbalimbali.Moja ya mbinu pekee
ambazo shetani anatumia ni kupitia uimbaji (MUZIKI) ili watu wamsifu au wapotoshane wao kwa wao na kuzama
kuzimu.
Kwa mfano katika miaka iliyopita
kuna mwimbaji aliimba wimbo mmoja usemao “IN
DEMON” yaani “NDANI YA SHETANI”.Katika
kipindi hicho wimbo huo uliteka watu wengi sana.Lengo lake kuu ni watu wawe
kwenye miliki yake(shetani).Ogopa
sana kumkaribisha shetani kwa jinsi hiyo kwenye Ibada yako siku zote.
Kumbuka mfalme Herode alikuwa ni mtu aliyempenda
sana Yohana mbatizaji lakini katika sherehe yake baada ya kupigwa mziki( nyimbo za kidunia ) na binti yake
kucheza sana akaingia kufanya maamuzi kinyume na mapenzi ya Mungu na yeye
mwenyewe ya kumkata kichwa Yohana mbatizaji.Hii ni kutokana na uwepo wa
kishetani uliokuwa umejaa pale kwa sababu ya nyimbo zile.
FAIDA
ZA SIFA YA KIMUNGU.
i).Kufunguliwa na
kuachiliwa huru.
Wakati ule Paulo na
Sila walipokuwa wakihubiri INjili kwa nguvu sehemu nyingi na kufanya miujiza ya
pekee hasa walipomfungua Yule kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo la utambuzi,
walikamatwa kwa kuteswa na kufungiwa gerezani na wale walinzi wakaamriwa
wawalinde sana.Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila wakakumbuka siri
iliyomo katika kufanya ibada hususani katika eneo la kusifu, wakawa wakimwomba
Mungu na kumwimbia nyimbo za kusifu, na mara tetemeko kuu la nchi likatokea,
Gereza nalo likatikisika wakati huo vifungo vya wote vikalegezwa na milango
ikafunguka.Matendo ya mitume 16:16-35.
Huu
ni ukweli usiopingika, nakumbuka kuna wakati ambapo tulikuwa tunaomba kwa ajili
ya watu watatu ambao walikuwa wamefungwa na nguvu za giza kwa namna mbalimbali
ndipo Mungu akaniambia niache kuomba nianze kusifu.Nilipoanza kusifu
nilijishangaa kuona kwamba nikiimba nyimbo hata ambazo sijawahi kuzisikia
mithili ya mtu anenaye kwa lugha, nikazidi kupata bubujiko ndipo wale watu
wakaanza kufunguliwa kwa namna ya ajabu sana isivyotegemewa.
Kuna wakati
mwingine unakuwa na vifungo mbalimbali katika maisha yako, unaona akili ni
nzito na huwezi kutatua matatizo au magonjwa mbalimbali labda watoto wako
hawafanyi vizuri katika masomo yao na umekata tamaa.Nakusihi hebu ingia kumsifu
Mungu na utaona maajabu ambayo haukutegemea.
ii).Kuta za Yeriko zinaondoka
katika maisha yako.
Katika mfululizo au
hatua ya kumiliki kwa wana Israeli nchi ambayo walikuwa wamepewa na BWANA kuna
wakati wakiendelea na safari Mungu aliwaonesha mji wa Yeriko na kuwapa.Lakini
haikuwa rahisi kama unavyoweza kufikiria kwani ule mji ulikuwa umefungwa kabisa
na kuzungushiwa ukuta mkubwa na imara.
Mungu akasema na Yoshua
na kumwambia, “……………………Nanyi mtauzunguka
mji huu, watu wote wa vita mkizunguka mji mara moja, fanyeni hivi siku
sita…………………..kisha itakuwa watakapopiga hizo pembe za kondoo waume kwa nguvu,
nanyi mtakaposikia sauti ya tarumbeta, watu wote watapiga kelele kwa sauti kuu;
na ukuta wa mji utaanguka chini palepale, na hao watu watapanda, kila mtu
akiendelea mbele kuukabili………………………”.Yoshua
6:1-20.
Sasa anaposema wapige
kelele kwa sauti kuu sio kwamba sauti yenye maneno yasiyo na maana ila watoe
sifa kwa nguvu sana kushangilia ushindi.Mahali pengine Biblia inasema, Msifuni
Mungu kwa kelele za shangwe.KELELE
ni sauti isiyo na mpangilio mzuri lakini maneno yatokayo kwenye hiyo sauti
yanakuwa na maana halisi.
Mara nyingi unapewa
maono mbalimbali ya vitu ambavyo umepewa na Mungu lakini ukitazama huvioni ila
unaona ukuta uliovizunguka.Pengine kuna kizuizi cha aina nyingine
kinachokufanya usipite na kuyakabili hayo maono.Ninakwambia, “ PIGA KELELE KWA SAUTI KUU” Umsifu Mungu,Lazima huo ukuta
utaanguka tu na hicho kizuizi kitatoka tu maana Mungu wetu ni Mungu ambaye
anafanya njia pale pasipokuwa na njia.Kama aliwavusha Israeli kwenye Bahari ya
Shamu uwe na uhakika hata katika mapito yako utavuka tu.Usimwache Shetani achukue
nafasi kwa kukudanganya na kukukatisha tamaa katika mawazo yako kuwa Mungu
hawezi.Yeye ni Alfa na Omega maana yake jinsi alivyofanya jana ndivyo
atakavyofanya leo na hata milele yote.Haleluya!!!
iii).Unajazwa kila kitu
unachokihitaji.
Duniani hapa wanadamu
wote ni wahitaji kwa namna moja au nyingine.Uhitaji ni hali ya kupungukiwa kitu
Fulani ambacho ni muhimu sana kwako.Inaweza ikawa ada ya shule, fedha ya
matumizi, usafiri, nyumba nzuri, chakula, nafasi ya kazi na mengineyo.Watu
wengi wameshindwa kupata vitu wanavyovihitaji kwa kukosea kitu hiki;
wanashindwa kusifu kikamilifu kwa vile wanakumbuka uhitaji wao badala ya
kumsifu Mungu bila kujali una uhitaji wa namna gani ili Mungu
akujaze.Nilikwambia usijaribu kutafakari ukubwa wa tatizo ulivyo wakati unasifu
bali tafakari ukubwa wa uweza wa Mungu juu ya hilo tatizo au uhitaji.
“Wanasimba hutindikiwa, huona njaa, bali wamtafutao BWANA hawahitaji
kitu chochote kilicho chema”.Zaburi
34:10.Hii haimaanishi kuwa hawatatumia vitu vyema.Maana yake hapa ni kuwa hata
kama watapungukiwa chochote wana sehemu ya kufanya viongezeke, kwenye kumcha
BWANA(katika sifa).
Kuna tofauti kubwa kwa
mtu Yule ambaye ameishiwa fedha ya matumizi na anayo ya leo tu na ya kesho
hajui ataipata wapi yaani anasubiri muujiza na yule ambaye ingawa ameishiwa leo
lakini benki katika akaunti anayo fedha ya kutosha mwaka mzima.Lazima huyu wa
pili hawezi kuhangaika au kupoteza muda wake kuanza kuombaomba kwa
majirani.
Wakristo wengi wamegeuka kuwa ombaomba kwa watu hata wasiomjua Mungu(wapagani) kwa sababu wameshindwa
kutulia na kumsifu Mungu ili awajaze kile wanachokihitaji.Matokeo yake
wameingia kwenye gharama ya kupokea vitu kimikataba
au kimaagano ambayo ni ya shetani au
pengine kupokea vitu ambavyo vimetolewa sadaka kwa miungu, mizimu au
kafara.Hebu acha kuwa ombaomba na kumwaibisha Mungu,Mpendwa wa BWANA!! Kumbuka
Mungu anacho kila unachohitaji hivyo jukumu lako ni kugeuka na kuanza kumsifu
na kumshuhudia Mungu kwa mambo makuu anayoyatenda na hakika atakupa unachokihitaji.Hata
kama unasumbuliwa na ugonjwa Fulani hebu uambie kwa imani tulia kimya niweze
kumsifu Mungu halafu anza kumsifu Mungu kwa moyo wako wote hakika Mungu
atatenda.
iv)Unapewa kushinda na
zaidi ya kushinda.
Sifa inatumika pia kama
moja ya silaha kuu ya kiroho.Kumbuka vita vyetu kama watu tuliookoka ni vya
rohoni kwa sababu maadui tunaopambana nao wapo katika mfumo wa roho katika
ulimwengu wa roho maana yake silaha tunazopaswa kuwa nazo ni za rohoni(2wakorintho 10:3-5).Mara nyingi Mungu
alipokuwa anawatuma watu wake kwenda kupigana vita silaha kuu aliyowaambia
kuitumia ni sifa.Ndivyo ilivyokuwa hata kwa wana wa Israeli kabila la Yuda
wakati wanaongozwa na mfalme Yehoshafati.
“naye
alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA na
kusifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi na kusema,Mshukuruni
BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele.Nao walipoanza kuimba na kusifu,
BWANA akawaweka waviziao juu ya wana wa Amoni na Moabu, na wa mlima Seiri,
waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa”.2Mambo
ya nyakati 20:21-22.
Na ukisoma sura yote
utaona kuwa ilifikia maadui wakaanza kuuana wenyewe kwa wenyewe lakini sababu
yake ni sifa.
Ndugu yangu usione
maadui wanakuja mbele yako halafu ukaanza kupiga mahesabu ya kujisalimisha hebu
piga kelele sema, “NAMSHUKURU BWANA KWA
MAANA FADHILI ZAKE NI ZA MILELE”.
Nakuambia iwe wachawi, mizimu, mapepo,
majini, waganga wa kienyeji au aina yoyote ile ya mateso hata ya kimwili njaa,
magonjwa, ukame, na adui yoyote Yule, usiogope.Maana Mungu wetu hataki kuaibika
na unapomsifu juu ya ukuu wake mbele za adui ndipo anataka ajioneshe kwa adui
uhalisia wa kile kinachotamkwa na wewe kupitia sifa zako, atakupigania nawe
utanyamaza kimya.
“Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa
yeye aliyetupenda”.Warumi 8:37.Ushindi
wako hautakuwa wa kawaida utakapochukua hatua ya kumsifu Mungu sawasawa.Tamka
mafanikio katika BWANA hata kabla ya
kuona mafanikio.Tamka lolote jema ambalo unaamini lipo mbele yako hata kabla
hujaliona Mungu akupendaye atakapoiangalia hiyo sifa yako lazima atakujibu tu.
Comments
Post a Comment